Jumamosi 17 Oktoba 2026 - 09:50
Ukimya wa Nchi za Kiislamu Dhidi ya Uhalifu wa Israel Umesababisha Vita Kupanuka

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi amesema kuwa ukimya wa nchi za Kiislamu mbele ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni umewapa viongozi wa utawala huo ujasiri zaidi wa kuendelea na vitendo vyao, kiasi kwamba wigo wa vita umepanuka kutoka Ghaza na kufika Lebanon, Iran na Yemen.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi, mkuu wa Harakati ya Uamsho wa Umma wa Mustafa nchini Pakistan na mkurugenzi wa Hawza ya Al-Urwatul-Wuthqa mjini Lahore, katika khutuba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika Msikiti wa Baitul-Atiq, jijini Lahore, huku akizungumzia uhalifu wa Israel huko Ghaza, alisema: Waislamu wanaodhulumiwa wa Ghaza wameziomba mara nyingi nchi za Kiislamu zenye uwezo wa kijeshi ziwasaidie, lakini hakuna hatua ya vitendo na yenye ufanisi iliyochukuliwa ili kusimamisha uhalifu wa Israel. Hali hii ya kutojali ilifikia kiwango cha kushangaza kiasi kwamba hata pendekezo la kuwapatia wahusika wa uharibifu wa Ghaza Tuzo ya Nobel lilitolewa; jambo ambalo, kwa mujibu wake, ni la kuaibisha.

Aliongeza kuwa; ukimya wa nchi za Kiislamu mbele ya vitendo vya uchokozi umewapa wavamizi ujasiri zaidi wa kuendelea na hatua zao. Matokeo yake ni kwamba wigo wa vita umepanuka kutoka Ghaza na kufika Lebanon, Iran na Yemen. Lengo la kushambulia maeneo haya na kuweka vizuizi vya kuwazingira ni kudhoofisha na kuangamiza safu ya Muqawama.

Mkuu wa Harakati ya Uamsho wa Umma wa Mustafa nchini Pakistan, huku akisisitiza nafasi ya Yemen katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, alisema: Kosa pekee la Yemen ni kwamba imechukua hatua za vitendo katika kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza na Palestina. Hali hii inajiri wakati ambapo nchi hiyo yenyewe imekuwa ikikabiliana kwa miaka mingi na vita, uharibifu na migogoro mikubwa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alitaja kuwa jitihada za kuchochea hisia za umma kwa kutumia jina la Haramain Sharifain (Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka na Madina), pamoja na kuzidisha mivutano ya kimadhehebu nchini Pakistan, ni hatua yenye hatari kubwa sana.

Alisema: Idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaunga mkono suala la Palestina na muqawama dhidi ya uchokozi wa Israel. Hata hivyo, baadhi ya makundi ya Takfiri, Nasibi na mashirika yaliyopigwa marufuku yanajaribu kutumia utambulisho wa Wasunni ili kutimiza malengo yao yenye nia ovu.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi alisisitiza kuwa; vita vinavyoendelea nchini Yemen na Iran hatimaye vitafikia mwisho. Lakini iwapo moto wa tofauti za kimadhehebu utawashwa nchini Pakistan, madhara yake yanaweza kuendelea kuikabili nchi hiyo kwa miongo kadhaa, kama ilivyokuwa katika vita vya Afghanistan.

Akizungumzia changamoto za kiusalama na kisiasa zinazoikabili Pakistan, aliongeza kuwa; nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na ukosefu wa usalama na ugaidi katika maeneo ya Balochistan na Khyber Pakhtunkhwa, migogoro ya kisiasa, ukosefu wa utulivu wa ndani na vitisho vinavyotokana na makundi yanayoitwa Fitnatul-Khawarij.

Kwa sababu hiyo, alisema kuwa badala ya kujiingiza katika migogoro ya kikanda, serikali inapaswa kutoa kipaumbele katika kutatua matatizo ya ndani na kudumisha utulivu wa nchi.

Katika kuendelea na hotuba yake, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi alimtaka Waziri Mkuu wa Pakistan, ajiepushe na matamshi ya uchochezi yanayotolewa kwa kutumia jina la Haramain Sharifain. Aidha, alisisitiza kuwa masuala nyeti ya kikanda yanapaswa kushughulikiwa kupitia diplomasia, mawasiliano rasmi kwa njia ya barua na mazungumzo, badala ya kuchochea hisia za wananchi.

Akizungumzia uhusiano kati ya Saudi Arabia na Yemen, alisema: Msaada wa kweli kwa Saudi Arabia haumaanishi kuunga mkono mashambulizi zaidi dhidi ya Yemen. Badala yake, msaada huo unapaswa kudhihirika kupitia jitihada madhubuti za kuzikaribisha nchi hizo mbili, kusimamisha mashambulizi na kuondoa mzingiro dhidi ya Yemen.

Aliongeza kuwa; Pakistan inaweza kutoa huduma kubwa katika eneo hili kwa kutekeleza jukumu lenye manufaa katika kuleta amani kati ya Saudi Arabia na Yemen.

Mkuu wa Harakati ya Uamsho wa Umma wa Mustafa nchini Pakistan, mwishoni mwa hotuba yake, alisisitiza kuwa; maslahi ya kitaifa yanaitaka Pakistan isiruhusu amani na utulivu wake wa ndani kuhatarishwa kutokana na shinikizo za nje.

Alisema kuwa nchi hiyo inapaswa kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kufuata diplomasia yenye shughuli na ufanisi zaidi, na huku ikiendelea kujitahidi kuleta amani katika eneo hili, pia iendelee kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa.

Alibainisha kuwa katika mazingira haya nyeti, kudumisha mshikamano wa kitaifa, kukabiliana na uchochezi wa kimadhehebu na kutatua tofauti kupitia njia za kisiasa na kidiplomasia ni miongoni mwa mahitaji ya msingi kwa ajili ya kulinda usalama na maslahi ya Pakistan.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha